Wazee ni Hazina hivyo lazima tuwatunze, tuwalinde na tuwahudumie. Ni baraka kubwa sana kupata zawadi hii, tunaamini wazee bado wana akili na nguvu za kufanya shughuli za ujasriamali kujiingizia kipato badala ya kutegemea misaada kutoka mashirika mbalimbali kama HelAge. Hayo yamesemwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Col. Michael M. Ngayalina wakati akizindua Baraza la wazee leo asubuhi katika ukumbi wa Champanda ulioko wilayani hapa.
Wazee tumieni elimu ya ujasriamali mliyopewa na shirika la HelpAge International kutafuta maeneo ya kilimo, ufugaji hata kuunda vikundi vya wazee kumi ili kupata mkopo. Ni vema maeneo hayo yawe karibu ili iwe rahisi kutembelea kila siku hususani ufugaji wa nyuki kuhakikisha hakuna wadudu wanao haribu asali au kudhibiti uchomaji moto.
Mizinga ya nyuki iwe ya kisasa ili kuepuka uharibu wa mazingira kwa kukata miti ya kuchonga mizinga, aidha napenda kuwakumbusha wazee kuwalea vijana wenu katika maadili ya kufanya kazi ili wasiwe tegemezi baadae na kusubiri kurithi mali za wazazi ambazo hawakushiriki kuzitafuta. Alisema Mhe. Ngayalina.
Mwisho nawashukuru sana shirika la HelpAge International kwa misaada mnayoendelea kuwapatia wazee wetu wa wilaya ya Buhigwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mzee Wenderin Kilenza amesema sisi wazee hatutegemei misaada tu kutoka HelpAge bali tunajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali mfano ufugaji wa nyuki ambao hauhitaji nguvu kubwa sana, kilimo cha muhogo, maharagwe, matunda kama parachichi, nanasi kwa ajili ya kuuza matunda na juisi.
Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Buhigwe Ndg. Petro Mbwanji amesema kwa kushirikiana na shirika la HelpAge Intenational tumefanikiwa kutoa vitambulisho vya matibabu bure kwa wazee 1050 kati ya wazee 14993 wa wilaya ya Buhigwe ambapo tunaendelea kutoa vitambulisho vingine kwa wazee walio salia na tumeweka mabango yanayosema "Mpishe mzee atibiwe kwanza" katika zahanati na vituo vya afya, katika kituo cha afya Muyama na Janda tumetenga vyumba maalumu kwa ajili ya matibabu ya wazee. Alisema Mbwanji.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz