Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umezindua Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kipindi cha pili cha awamu ya tatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe leo Jumanne, 25 Mei, 2021 katika ukumbi wa kanisa la Anglikana Dayosis ya Western Tanganyika Buhigwe mnamo saa 4:00 subuhi.
Madhumuni ya Kipindi cha Pili ni kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa na kulinda maslahi ya watoto wao.
Kipindi cha Pili kitafikia malengo yake kwa kutekeleza shughuli mbali mbali kupitia sehemu kuu tatu ambazo ni uhawilishaji fedha ambao utaongeza kipato cha kaya na kuwekeza katika afya na elimu ya watoto, kuinua uchumi wa kaya kwa kujenga uwezo kwa kaya katika utunzaji rasilimali na kutengeneza njia mbadala na endelevu za ajira na kushiriki katika kazi za jamii na kupata kipato cha ziada kwa matumizi ya kaya kama chakula na kugharamia mahitaji mengine ya msingi na wakati huo wakiboresha miundombinu katika jamii na kupata ujuzi na stadi za maisha.
Hayo yamesemwa na Afisa Miradi ya Jamii TASAF makao makuu (Ndg. Henry Mbago) kwa niaba ya Mkurugenzi wa TASAF Tanzania wakati akisoma risala kwa Mgeni rasmi Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Col. Michael M. Ngayalina
Afisa Miradi ya Jamii TASAF makao makuu (Ndg. Henry Mbago akisoma risala kwa Mgeni rasmi
Aidha Ndg. Mbago aliongeza kuwa walengwa wa Mpango huu ni Kaya zinazoishi katika hali duni katika vijiji vyetu ambapo wanufaika ndani ya kaya ni watoto chini ya umri wa miaka mitano(5) wanaoenda Kliniki, Mama mjamzito na watu wenye ulemavu.
Katika Hotuba yake, Mgeni rasmi Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe ameagiza kwamba Pesa ya ruzuku ya TASAF kwa walengwa isiishie kula nyama choma na kulewa pombe isipokuwa zitumike kuibua miradi itakayo imarisha uchumi wa kaya mfano, ujasriamali, kilimo, ufugaji n.k
Kwa upande wa Viongozi na wataalamu waliohudhuria kikao kazi hicho, amewasihi kuwa mabalozi wazuri wa TASAF kwa kukemea vitendo vya udanganyifu wakati wa kuandikisha kaya mpya, wakati wa kubaini kaya duni na kwamba kila wanapofanya ziara za kikazi wazungumzie umuhimu wa TASAF.
Walengwa wakumbuke kuwa TASAF haitakuwepo siku zote, hivyo wajiwekee akiba kwa kufanya shughuli za kujipatia kipato.
Pia tuwapongeze walengwa wanaofanya vizuri kwenye matumizi ya ruzuku za TASAF na tuwakemee wale wanaotumia vibaya ruzuku hizo.
Niwatakie kila la heri katika kikao kazi hiki, kisha kusema hayo natamka rasmi kwamba kikao kimefunguliwa.
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Col. Michael M. Ngayalina (katikati), Kulia kwake ni Mhe. Venance Kigwinya, M/kiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, na kushoto mwa picha ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Ndg. Idrisa Naumanga.
Naye M/kiti wa Halamshauri ya Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Venance Kigwinya amemshukuru Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa hotuba nzuri na kuahidi kuyafanyia kazi yote yaliyoagizwa. Aidha amewapongeza waelimishaji ngazi ya Jamii, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wahe. Madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama (w) kwa kuhudhuria kikao hicho.
TASAF imetusaidia sana sisi viongozi hususani katika maeneo ambayo wananchi wanamaisha duni. Tunaahidi kuendelea kutoa elimu kwa walengwa ili ruzuku hizi wazitumie vizuri hatimaye kujikwamua kwenye wimbi la umaskini wa kipato, afya, elimu n.k
Mhe. Venance Kigwinya-Mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz