Mkuu mpya wa Kigoma Mheshimiwa Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye amefanya ziara ya siku mbili wilayani Buhigwe ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipofika katika Mkoa wetu wa Kigoma , katika ziara yake iliyoanza tarehe 1/9/2020-2/9/2020 Mhe. Andengenye alipata fursa ya kujitambulisha kwa wananchi wa wilaya ya Buhigwe , kukagua miradi ya maendeleo, kufanya mikutano ya hadhara na kutatua kero za wananchi.
Awali akizungumza na wananchi wa kata ya Munanila Andengenye amesisitiza mambo makuu manne, kwanza Wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya (Chf iliyoboreshwa) kwa kulipia shilingi 30000/= kwa kila kaya kwa mwaka mzima ambapo itamwezesha mwananchi kupata huduma za matibabu bure na kwamba Bima ya afya ni ufunguo wa kumuona Daktari, kupata vipimo na kuchukua dawa kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya afya na Hospitali, Pili wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo kwani serikali ya awamu ya tano inatenga kiasi cha Bilioni 24 kila mwaka katika kutekeleza mpango wa elimu bure, Tatu ni swala la Ulinzi na Usalama; lazima kila mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo mbalimbali vya dola kama jeshi la Polisi. Tusifiche wahalifu tutoe taarifa za kweli siyo za fitina, Nne Tunaelekea kwenye Uchaguzi mkuu, nitoe rai kwa wananchi wote wenye sifa za kupiga kura mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura ili kumchagua kiongozi unayempenda kwa maendeleo ya Taifa letu.
Kisha hapo Mhe. Mkuu wa Mkoa alielekea eneo kinapojengwa chuo cha VETA na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho kabla ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya wilaya, Shule ya Msingi Mji Mpya na Jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya Buhigwe, akikagua ujenzi wa bwalo la kulia chakula katika shule ya msingi Mji mpya Andengenye amesema ijengwe mifumo ya kung'amua moshi (smoke detector)na Fire extinguisher ili kuzuia hatari ya mlipuko wa moto.
Aidha akiongea na wananchi wa kata ya Munzeze Mhe. Mkuu wa Mkoa amewapongeza wananchi kwa shughuli za maendeleo hususani kilimo cha tangawizi, "niwahakikishie tu kwamba Serikali ya awamu ya tano imewaletea nishati ya umeme ili kujenga kiwanda cha kusindika tangawizi na hivyo tuanze kuuza tangawizi iliyochakatwa".Alisema Andengenye.
Mhe. Mkuu wa Mkoa Thobias Andengenye akizungumza na wananchi wa kata ya Munzeze wakati wa ziara yake wilayani Buhigwe.
Hata hivyo Andengenye alipata fursa ya kutembelea mradi wa maji unaojengwa katika kata ya Munyegera na kushiriki uchimbaji wa mtaro wa kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tanki la kijij.
Mhe. Andengenye akishiriki uchimbaji mtaro wa maji katika kata ya Munyegera wilayani Buhigwe wakati wa ziara yake leo.
Ziara iliendelea ambapo Mkuu wa mkoa na timu yake alielekea Shule ya sekondari Muyama na kukagua ofisi iliyojengwa kwa mradi wa EP4R na kutokuridhishwa na miundombinu ya ofisi hiyo ndipo alimwamuru Mhandisi wa Ujenzi wilaya Eng. Zacharia Ntambala kuhakikisha marekebisho ya sakafu na marumaru yanafanyika haraka. Baada ya hapo alielekea kijiji cha Kasumo kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara kabla ya kuelekea kijiji cha Migongo kuwasha umeme wa REA kwa kaya 12 za mwanzo.
Kwa upande wake Bi. Agneta Kmlenga ambaye ni miongoni mwa wananchi waliopata huduma ya umeme katika kijiji cha Migongo amesema "Naishukuru sana Serikali ya awamu ya tano kwa kuniletea umeme na nitautumia kwa kufanya ujasiriamali mdogomdogo kama kutengeneza juisi na kuuza ili kujipatia kipato, nitanunua jokofu, jiko la umeme, pasi na nitauza maji baridi".
Na mwisho kabisa Mkuu wa Mkoa alihitimisha ziara yake katika kata ya Mugera ambapo aliongea na wananchi katika mkutano wa hadhara na kuwashukuru mamia ya wakazi waliojitokeza kumpokea.
Mhe. Mkuu wa Mkoa Kigoma akikata utepe kuashiria kuwashwa kwa umeme wa REA katika kijiji cha Migongo. Picha na Alexander Michael@Information Officer Buhigwedc
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz