Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Kamishna wa Polisi Thobias Andengenie hivi karibuni amefanya ziara ya kukagua miradi ya UN Kigoma JOINT PROGRAMME iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kwa kutembelea kata nne (4) ambapo miradi hiyo imejengwa. Kata hizo ni pamoja na KINAZI, JANDA, MUYAMA na BUHIGWE.
Katika kata za Kinazi na Janda, amekagua viwanda vidogo vya kukamua Mawese vilivyojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Kituo cha Biashara Duniani (ITC) kupitia mradi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa Mkoa wa Kigoma (UN-KJP).
Mhe. Andengenie, amewahimiza wananchi kuongeza uzalishaji wa mafuta ya mawese ili viwanda hivyo vilete tija katika jamii inayowazunguka, kujenga uzio kuzunguka eneo la viwanda, kuandaa vifungashio kwakuwa vifungashio ndio kivutio cha macho ya wateja, kuandaa LEBO itakayotambulisha biashara yao ya mafuta ya mawese.
"Wito wangu kwa Afisa Biashara Mkoa na Maafisa Biashara wote, tuwe na duka letu ngazi ya mkoa linalotambulisha bidhaa zetu za mawese na endapo uzalishaji utaongezeka basi tutapanua soko kwa kufungua maduka mengine nje ya mkoa wetu wa Kigoma" Alisema Andengenie.
Mwisho aliwapatia akina mama zawadi ya Shilingi Milioni Moja baada ya kuvutiwa na usimamizi katika kuendesha viwanda hivyo.
Kwa upande wao, akina mama, walimshukuru sana Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara yake katani hapo na kumpatia zawadi ya Jogoo mwenye thamani ya Shilingi Elfu ishirini.
Akina Mama katika Kata ya Janda wakimkabidhi zawadi ya Jogoo Mhe. Mkuu wa Mkoa Kigoma, wakati wa ziara yake katani hapo.
Akiwa kata ya Buhigwe, Mhe. Andengenie, alitembelea jengo la Vijana ambalo pia limejengwa kwa hisani ya UN-KJP na kuzungumza na watumishi wa ummma na baadhi ya vijana waliohudhuria ziara hiyo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ndg. Christopher Kajange akisoma taarifa ya mradi wa Jengo la vijana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa Kigoma.
Ziara ilihitimishwa kwa kutembelea Soko la Muyama, ambapo ujenzi unaendelea na utarajia kukamilika mwezi Julai, 2021.
Soko la Muyama katika hatua ya kupandisha ukuta.
Imetolewa na Kitengo cha Tehama, Ofisi ya Mkurugenzi, Mji wa Bwega, P.o.box 443,-Buhigwe.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz