Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na Watoto Mhe. Mwanaid Ali Khamis (MB) ametembelea na kushiriki ujenzi wa Zahanati ya Kibuye Kata ya BUKUBA wilayani Buhigwe Pamoja na kujionea maendeleo ya Ujenzi wa Kiwanda kidogo cha kuchakata zao la chikichi (Uzalishaji wa mafuta ya MAWESE) cha akina mama cha NYAMUNINYA.
Awali katika kushiriki zoezi la ujenzi wa Zahanati ya Kibuye, akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imefikia hatua ya Linta, Mtendaji wa Kijiji hicho alisema Gharama za ujenzi wa Zahanati hiyo hadi kufikia hatua hiyo ni Tsh 14,238,600 ambapo fedha hizo ni nguvu ya wananchi na halmahsauri ya wilaya. Aliongeza kuwa jumla ya gharama za ujenzi huo hadi kukamilika ni Tsh 65,000,000 na kumuomba Mh Naibu kuchangia na kutia mkazo kiasi kinachobaki kupatikana kutoka serikalini ili kukamilisha boma la zahanati hiyo. Taarifa ya mtendaji huyo iliongeza kuwa ari ya wananchi ilikuja baada ya kupata adha za kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya kwenye kata ya Jirani ya Janda.
Katika kujibu taarifa ya ujenzi Mhe. Naibu Waziri alichangia papo hapo Tsh Laki 5 na kuahidi kufikisha ombi la fedha zinazobaki kwa serikali. Aliendelea kwa kuwashukuru wananchi kwa moyo wa kujitolea na kusisitiza kuendelea kutumia rasilimali zinazowazunguka kutimiza malengo ya maendeleo.
Katika kuhitimisha hotuba yake eneo la kwanza akishiriki ujenzi wa Zahanati alisisitiza wanachi kuendelea kuchukua Tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19 na kukemea vikali unyanyasaji wa kijinsia kwa akina mama na Watoto na kuwataka kutokukaa kimya pindi matendo hayo yanapofanywa juu yao au kwa Watoto wao.
Awali kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Kanali Michael Ngayalina alisisitiza kuwa bima Afya ni muhimu na ametia hamasa kwa kumuongezea Tsh 5,000 kwa kila mwananchi atakayehitaji bima ya afya. Katika hotuba yake Naibu Waziri aliungana na Mkuu wa wilaya hiyo kusisitiza kuwa magonjwa hayana hodi huja wakati wowote hivyo bima ya Afya ni mkombozi sahihi.
Upande mwingine wakati akijionea ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata mazao ya Chikichi (Kuzalisha mafuta ya MAWESE)-cha Akina mama Nyamuninya, Naibu Waziri amekipongeza kikundi hicho, uongozi wa Kijiji, halmashauri na wadau wa maendeleo kama ITC na SIDO (kupitia mradi wa Pamoja wa Kigoma (KJP) kwa ubunifu wanaofanya kuongeza viwanda hasa vinavyomilikiwa na vikundi vya akina mama.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho kwa niaba ya wanakikundi wa Nyamuninya Mtendaji wa Kijiji alisema Gharama za ujenzi huo ni Tsh 57,641,620 ambapo Mchango wa ITC na SIDO kupitia mradi wa Pamoja KJP ni Tsh 56,525,000/= na kikundi kilichangia 1,116,620. Katika kutia chachu ya ykamilishaji Naibu Waziri alikipa kikundi Tsh Laki 1
Katika kuhutimisha hotuba yake Naibu Waziri alipigilia msumari kwa kuwataka wanawake kutokaa kimya kwa aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia kwao au kwa Watoto wao na kuwataka kuwa tayari kutoa Ushahidi pale wanapohitajika
Naibu Waziri pia aliwataka vijana kuchangamkia asilimia nne za halmasahuri za vijana kujiletea maendeleo kwa kuanzisha miradi kukuza kipato
Awali Mwenyekiti wa CCM wilaya alipopewa nafasi kabla ya Naibu Waziri kuhotubia alimshukuru na kutuma salamu kwa Mhe. Makamu wa Rais na Mhe. Rais huku kilio cha watumishi wilayani hapo akimtwika Naibu Waziri kulitizama kwa jicho la tatu.
Mwisho Diwani wa kata hiyo Alimshukuru Waziri kwa wito na moyo kwa yote aliyofanya na kusisitiza kuwa shughuli za maendeleo katani kwake zinaenda kwa kasi na kumkaribisha tena Bukuba.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz