Maafisa Ugani kutoka kata za Kibwigwa, Mugera, Biharu, Muyama na Munyegera Wilayani Buhigwe wameaswa kutumia Pikipiki hizo kwa ajili ya kuwasaidia Wananchi ili kuinua sekta ya kilimo kwa kutoa elimu kwa vitendo juu ya kilimo cha kisasa, hivyo wametakiwa kutumia Pikipiki hizo kwa weledi mkubwa, kwa kuzingatia sheria za barabarani na kuleta matokeo chanya kwa wakulima katika kata zao.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Mhe. Luteni Canal Michael Masala Ngayalina amesema hayo leo katika zoezi la ugawaji wa pikipiki lililofanyika mbele ya Ofisi yake ambapo amewataka maafisa ugani hao kutumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
“Nawataka mtambue kuwa nyie ndio mabalozi wa Kilimo katika kata zenu, na balozi mzuri ni yule anayezingatia weledi na kutimiza wajibu wake kwa kufuata misingi ya Sheria, Kanuni na Taratibu akitambua yeye ni kioo cha wale anaowahudumia. Ukiona wewe huwezi kutimiza wajibu wako kwa kufuata maadili basi serikalini sio sehemu sahihi kwako ni vyema ukatafuta pahali pengine” alisema Ngayalina.
Ngayalina aliongeza kuwa utofauti wao na watu wengine uonekane katika maadili yao ya kiutendaji ikiwemo uwajibikaji, kujali muda, kuwasaidia wananchi, kuanzisha shamba darasa, ,ubunifu, kuwasikiliza wakulima na kuheshimu Sheria ili wale wanaowahudumia watamani kufanya kazi ya kilimo.
Kwa upande wao maafisa ugani hao waliishukuru msaada huo wa kupatiwa usafiri kuweza kuwafikia wakulima mara kwa mara jambo linalochangia kutoa nafasi ya kujadili changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wadau wa kilimo na kwa manufaa ya Taifa.
“Kwa kweli mimi binafsi nimefaidika na mambo mengi ambayo Mhe. Mkuu wa Wilaya ametuasa katika hafla hii ambapo naamini mimi na wenzangu tutaendelea kujituma kwa kuzingatia misingi katika utendaji wetu, hasa kwa kuanzisha mashamba darasa maana ni kama ulivyosema sekta ya kilimo inatoa huduma na elimu kwani wakulima wengi tunaowahudumia ni vijana na wazee wanaotuangalia utendaji wetu, endapo tutafanya kinyume cha maadili yetu hata wao watakosa maadili na ari ya kufanya shughuli za kilimo” alichangia mmoja wa maafisa ugani.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz