Katika kuadhimisha siku ya lishe kitaifa Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe wamesisitizwa kutumia Vyakula vyote mchanganyiko kutoka makundi sita ya vyakula kwa ajili ya kudumisha Afya zao.
Hayo yamesemwa na Mh Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe,Kanali Michael Ngayalina wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Lishe kitaifa ambayo kwa ngazi ya Wilaya yamefanyika katika kijiji cha Kibuye kata ya Bukuba.
Aidha ameongezea kwa kusema kuwa suala la lishe ni la watu wote na kuwasisitiza Wazazi na Walezi kuchangia chakula kwa ajili ya watoto kupata chakula wanapokuwa mashuleni na kuwaasa Wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kwenda vituoni kupiga Kura mnamo tarehe 27 Novemba 2024.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe amesema kuwa shughuli za maadhimisho hayo ni kwa ajili ya kutoa Elimu na kuhamasisha suala la Lishe kwa maslahi mapana ya Wilaya na nchi kwa Ujumla na kutumia Elimu hiyo iliyotolewa na Wataalamu kwa ajili ya kuboresha afya za watoto wao na familia kwa ujumla.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Dkt Innocent Mhagama amesema kuwa Elimu ya Lishe inatolewa kwa njia mbalimbali katika jamii ikiwemo kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya lakini pia kupitia watoa huduma kwa ngazi ya jamii.
Kwa mwaka wa 2024 Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu inayosema “Mchongo ni Afya yako,Zingatia unachokula” na kwa Wilaya ya Buhigwe yameadhimishwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo Elimu ya Afya,utoaji wa Matone ya Vitamin A,jiko darasa la mafunzo ya kuandaa chakula bora cha watoto kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo ya Buhigwe,huduma za Uzazi wa mpango,Malaria na Upimaji wa hali ya lishe na Pia watoto walipata nafasi ya kulishwa chakula hicho ambacho walikifurahia sana.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz