Mh Kanali Michael Ngayalina ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe ameagiza Watendaji wa Kata zilizofanya vibaya kwenye utoaji wa chakula Mashuleni katika kipindi cha Julai-Septemba 2024 kuongeza ubunifu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula ili kufikia lengo la kuondoa udumavu na kuongeza upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi wilayani humo.
Kata zilizofanya vibaya ni pamoja na Janda,Mugera,Buhigwe,Kibande,Munyegera na Rusaba ambazo amezitaka kuondoka kwenye mstari mwekundu kwa kushiriki kwa vitendo kufikia lengo la Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassani la kumaliza tatizo la lishe nchini.
Ameyasema hayo leo tarehe 23 Oktoba wakati akipokea taarifa ya Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023-2024 pamoja na tathmini ya Viashiria vya Mkataba wa lishe ambapo pia amezipongeza kata za Mkatanga, Kibwigwa, Kinazi, Kilelema pamoja na Biharu kwa kufika zaidi ya nusu ya lengo la la utoaji wa chakula mashuleni.
Aidha ameongeza na kuzitaka shule zote wilayani humo kupanda miti ya Matunda kwenye mipaka ya shule hizo na kuagiza ofisi za watendaji kupanda miti ya matunda kwenye ofisi zao.
Sambamba na hilo ameiagiza Divisheni ya Kilimo kuwezesha Shule zote kupata mbegu ya viazilishe haraka kwa ajili ya kupandwa wakati huu unapoanza msimu wa mvua.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Ndugu George E Mbilinyi amewaasa watendaji hao kuwa wa mfano katika kukabiliana na tatizo la lishe ikiwemo kutoa lishe bora kwa wanafunzi na familia zao kwa ujumla.
Naye Afisa Lishe Wilaya ya Buhigwe Melina Jombe amesema kuwa kitengo cha Lishe Wilaya ya Buhigwe kimekuwa kikitekeleza Viashiria 23 vya Lishe,Vikiwemo viashiria 9 kutoka Chama tawala (CCM) na vyote vimekuwa vikifanya vizuri ingawa kuna kata chache bado zinalega.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz