Wananchi wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, wamejitokeza kwa wingi kumlaki Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa (MB) na kuiomba Serikali ya awamu ya tano kusaidia kutatua changamoto za kilimo hasa kwa mazao ya Kahawa, Tangawizi na Michikichi ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini pia kujiajiri katika sekta ya kilimo na kuchangia ukuaji wa Tanzania ya Viwanda.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Mheshimiwa Brig. Generali Marco E. Gaguti kwa niaba ya wananchi wakati akisoma taarifa ya wilaya mbele ya Waziri Mkuu wakati wa ukaribisho wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani hapa.
Akijibu taarifa hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji kutatua changamoto hiyo.
“Nakuagiza Waziri wa Kilimo simamia tozo zote ambazo hazina tija katika mazao haya ili kuwasidia Wananchi na nipate majibu haraka.”Alisema Waziri Mkuu.
Mhe.Kassim Majaliwa alitumia fursa hiyo kuhamasisha kilimo cha zao la Michikichi huku akiwaagiza Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Afisa Kilimo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha miche ya michikichi inaoteshwa kwenye vitalu na kupandwa shuleni, kila mwananchi na kando ya barabara ikiwa kuna udongo wenye rutuba.
Pia Mhe. Waziri Mkuu ameweka jiwe la Msingi katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe.
Aidha Waziri Mkuu, ametoa rai kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha mipaka yote ya wilaya inalindwa ili kudhibiti wahamiaji haramu.
“Wilaya ya Buhigwe iko mpakani mwa nchi jirani ya Burundi, hivyo jeshi la Polisi hakikisheni mipaka yote ya Halmashauri inalindwa, na kila mhamiaji lazima afuate utaratibu.” Aliongeza Mhe. Kassim Majaliwa.
Mwisho aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Buhigwe na Wananchi wake kwa mapokezi na ushirikiano mzuri waliouonyesha wakati wa ziara yake Wilayani hapa.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz