Serikali imeandaa mkakati wa kuboresha sekta ya mifugo pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo huku ikiwahimiza wafugaji kuzingatia matumizi ya majosho yenye dawa.
Akizungumza na wafugaji, Afisa Mifugo na Uvuvi Wilayani Buhigwe Ndg. Lichard Kayoka wakati wa zoezi la uhamasishaji wa uogeshaji wa ngo’mbe kanda ya Magharibi Mkoani Kigoma, katika kijiji cha Kigege kilichopo kata ya Biharu Halmshauri ya wilaya ya Buhigwe amewataka wafugaji kufanya zoezi la uogeshaji wa mifugo ulioanzishwa uwe wenye tija na endelevu, kwa vile hivi sasa hakuna sababu za kushindwa kuogesha mifugo yao katika majosho yenye dawa ya kudhibiti kupe.
Aidha amesema kuwa kwa sasa serikali katika zoezi hili, imetoa dawa bure kwa Halmashauri zote nchini, na kukarabati majosho yote yaliyokuwa hayafanyi kazi, ili wafugaji waweze kuogesha mifugo yao , kukinga ugonjwa hatari unaoenezwa na kupe, ambao unaongoza katika vifo vya ng’ombe hapa nchini.
“Mwanzo shughuli hizo zilikuwa zikifanywa kwa ,kutofuata taratibu nzuri na makusanyo yalikuwa yakitoka kwa wafugaji walipokuwa wakipata huduma za kuogesha mifugo yao, hazikuwa na taarifa ya mapato na matumizi na hivyo kushindwa kuwa na utaratibu endelevu wa shughuli hiyo, majosho mengi yalisimama kufanya kazi”amesema Kayoka.
Katika kampeni hii ya uhamasishaji wa uogeshaji wa mifugo tozo imepungua ambapo hivi sasa kila ng’ombe ana ogeshwa katika majosho ni shilingi 50 tu, huko nyuma uogeshaji ulikuwa unatozwa wastani wa shilingi mia mbili (200/=) kwa kila ngo’mbe na kwa mbuzi ilikuwa shilingi kumi (10/=).
“Nyie wafugaji msikalie raslimali hii ya mifugo mliyokuwa nayo, kwani ni kitega uchumi kikubwa sana mlichonacho”amesisitiza Kayoka.
Aidha alifafanua ufugaji kwa kufuata taratibu za ufugaji wa kisasa na kibiashara kwa kuvuna mifugo inapozidi katika eneo ulilokuwa nalo, itakusaidia kupata kipato katika kuboresha maisha yako na ya familia.
Uhamasishaji huu unafuatia uzinduzi wa kampeni ya uogeshaji wa mifugo,iliyofanywa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina katikati ya mwezi jana katika kijiji cha Buzirayombo Halmashauri ya Chato.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz