WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum) George Mkuchika amewasihi Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe na watanzania kwa ujumla kulinda amani,umoja na ushirikiano uliopo baina yao.
Hayo ameyasema leo tarehe 04 mwezi April 2025 wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe alipotembea mradi wa ujenzi wa Tenki la maji linalogharimu kiasi cha Shilingi Bil 9.7 unaotegemewa kukamilika mwaka huu 2025 June ambao tayari umeshaanza kuhudumia Wananchi katika ziara ya kikazi ambayo ameifanya katika mkoa wa Kigoma.
“Ndugu zangu wa Buhigwe,maendeleo kama haya yanafanyika kwasababu Nchi yetu ina amani,kama Nchi haina amani hatuwezi kufanya chochote,Nawaomba Watanzania wenzangu tuitunze amani tuliyonayo kwa gharama yoyote”Amesema Kapteni Mkuchika
Aidha amewasisitiza Wananchi kujitokeza kwa wingi katika vyombo vya usalama kufichua wale wote watakaoona wana nia ya kuchafua amani ya nchi yetu.
Kwa niaba ya mkoa wa Kigoma,Mkuu wa Mkoa huo Thobias Andengenye amesema kuwa kwa mkoa wa Kigoma wamepokea fedha nyingi kutoka Serikalini ambazo zimewasaidia kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo Shule,Barabara,maji na Hospitali.
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amemshukuru Waziri Mkuchika kwa ujio huo pamoja na rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania Rais Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 kwa ajili ya ujenzi wa tenki hilo la maji ambalo litaenda kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa Wilaya ya Buhigwe.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Venus Kigwinya amesema kuwa Wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kuwapatia fedha ambazo zimewawezesha kupata miradi mbalimbali ikiwemo hospitali ya Kisasa ya Wilaya ya Buhigwe.
Kwa upande wao Wananchi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia fedha ambazo zinajenga tenki hilo la maji na kutatua kero ya maji ambayo ilikuwa inawasumbua hasa katika kipindi cha kiangazi.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz