Tarehe 31Oktoba 2017 Timu ya Wataalamu kutoka Ofis ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Buhigwe ikiambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ( Mhe. Venance Kigwinya) walishiriki hafla fupi ya uzinduzi wa soko la Mpakani katika kijiji cha Nyamugali, ambapo wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani walishiriki uzinduzi huo. Soko hilo litahusisha biashara kati ya nchi jirani ya Burundi na wananchi wa vijiji vilivyoko mpakani baina ya nchi hizi mbili yaani Tanzania na Burundi na hivyo kuongeza mapato kwa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Taifa kwa ujumla. Aidha soko hilo litasaidia kuinua fursa za uchumi, ujasiriamali, uwekezaji, upatikanaji wa huduma za kijamii, uhusiano mwema na kuleta maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na hatimaye kupunguza wimbi la umaskini.
Soko la mpakani Nyamugali wilayani Buhigwe ambalo liko takribani umbali wa mita za mraba (400-600) kutoka mto Maragarasi ambaokimsingi ndio mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Burundi.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nyamugali Ndg. Athumani Amani Mulinga aliwakaribisha wataalamu kutoka Ofis ya Mkurugenzi Mtendaji wilaya ya Buhigwe, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Diwani wa kata ya Nyamugali na kuanza utambulisho mbele ya wananchi wa kijiji cha Nyamugali walio hudhuria ufunguzi wa soko hilo kisha akatoa historia fupi kuhusu ujenzi wa soko hilo mpaka kukamilika kwake.
Kutoka kulia mwa picha ni Mchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe (Ndg. Said Lue) akifatiwa na Afisa Mtendaji kijiji cha Nyamugali (Ndg. Athumani Amani Mulinga), Mwenyekiti wa Halmashauri wilaya ya Buhigwe (Mhe. Venance Kigwinya), Afisa Biashara wilaya (Ndg. John Onesphory) kisha Mheshimiwa Diwani wa kata ya Nyamugali
Mwenyekiti wa Halmashauri aliwaasa wananchi wa kijiji cha Nyamugali kilichomo wilayani humo kuchangamkia fursa za biashara kwakuwa soko hilo liko mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Burundi, hivyo biashara itahusisha nchi hizi mbili. Aidha wananchi hawataruhusiwa tena kupeleka mazao yao nje ya nchi na kutafuta soko kama ilivyokuwa awali badala yake watauzia bidhaa zao ndani ya nchi kwakuwa sasa soko limezinduliwa rasmi na ni halali kisheria. Mfanya biashara atakaye kamatwa amepeleka kuuza bidhaa zake nje ya nchi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, mwisho alisisitiza kuhusu utunzwaji wa soko hilo kwa kufanya usafi na kulinda miundombinu yake kwa ujumla.
Wananchi wa kijiji cha Nyamugali wakisikiliza kwa makini ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na jopo la wataalamu kutoka Ofis ya Mkurugenzi wa wilaya ya Buhigwe.
Mji Mpya wa Bwega-Ofisi za Mkurugenzi
Postal Address: P.O.Box 443 Buhigwe
Simu Ya Mezani: 0282988460
Simu ya mkononi: (+255) 782 500 333
Barua Pepe: ded@buhigwedc.go.tz